Friday, 17 June 2016

Simu bandia kwaheri!

Nusu ya bidhaa nchini ni feki, siyo simu tu!!!

Dar es Salaam.Wakati simu feki zikiwa zimezimwa usiku wa kuamkia leo, imeelezwa kuwa nusu ya bidhaa mbalimbali zinazotumika nchini zikiwamo dawa za binadamu ni feki.

Imeelezwa kuwa asilimia 50 ya bidhaa hasa dawa za binadamu na vifaa vya umeme havina sifa, hivyo kuhatarisha maisha ya watumiaji wake.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi katika utafiti alioufanya kuhusu tatizo la bidhaa feki nchini na kudhaminiwa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Utafiti huo, alisema uliwashirikisha watumiaji wa bidhaa 250 na kampuni 47 zinazotengeneza bidhaa mbalimbali nchini.

“Nusu ya bidhaa zilizoko sokoni ni bandia, dawa za binadamu na vifaa vya umeme ni miongoni mwa bidhaa hizo; unaweza kuona namna hali ilivyo mbaya kwa maisha ya binadamu,” alisema.

Alisema watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya bidhaa bandia na bidhaa halisi, kwa sababu ya uelewa mdogo.

“Katika jamii yetu wako wanaotumia dawa bandia na hawaponi magonjwa wanayoumwa na wengine kufunga vifaa bandia vya umeme kwenye nyumba zao na kusababisha ajali za moto, mambo haya yanaweza kuleta maafa,” alisema.

Profesa Ngowi alisema wako wanaonunua bidhaa hizo kwa sababu ya umaskini.

“Baadhi wanazifahamu bidhaa halisi, lakini wananunua za bandia kwa sababu ya kutokuwa na uwezo,” alisema.

Akitoa mfano kwa wauzaji wa vipuri vya magari, Ngowi alisema wamekuwa wazi kuwaeleza wateja kuwa wanauza bidhaa bandia na bidhaa halisi.

“Hapo mnunuzi unachagua ununue bidhaa halisi ambayo bei yake ni kubwa au ununue bidhaa bandia, ambayo bei yake ni ndogo,” alisema.

Serikali yakosa mapato

Alisema Serikali inakoseshwa mapato kwa sababu waingizaji wa bidhaa bandia hawalipi kodi, kwa vile zinaingizwa nchini kwa kutumia njia zisizo rasmi.

“Nchi yetu ni kubwa yenye njia nyingi zisizo rasmi ambazo bidhaa hizo zinapitishwa, wakati umefika kwa Serikali kuweka mikakati ya kuzizuia,” alisema.

Alipendekeza Serikali kuongeza udhibiti katika njia zisizo rasmi na kushirikiana na kampuni zinazozalisha bidhaa, kuwaelimisha wananchi ili waweze kutambua bidhaa halisi na bidhaa bandia.

Alisema Serikali inatakiwa kuongeza vituo vya ukaguzi kwenye njia zisizo rasmi ili kudhibiti bidhaa hizo.

Alisema nchi ambazo ni maarufu kwa uingizaji bidhaa bandia nchini ni China, India, Indonesia, Taiwan, Singapore, Malaysia, Thailand, Chile, Afrika Kusini, Kenya, Msumbiji na Malawi.

Akichangia kuhusu utafiti huo, Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Ushindani nchini (FCC), Braise Freedom alisema tume hiyo imekuwa ikitangaza kuhusu bidhaa feki kupitia vyombo vya habari.

Alisema kampuni zinatakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu bidhaa mbalimbali wanazozitengeza ili waweze kuzitofautisha na bidhaa feki.

Kwa upande wake, Mtafiti Ellis De Bruijin wa kampuni ya Compol Associates Ltd ya jijini Nairobi, alisema tatizo la bidhaa feki lipo katika sekta nyingi nchini.

Akitoa mfano, alisema hata baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa habari ambazo si za kweli na kwamba hali hiyo ni sawa na uzalishaji wa bidhaa feki.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CTI, Evarist Maembe alisema wametoa udhamini wa utafiti huo ili shirikisho hilo liweze kupata mapendekezo na kutoa ushauri kwa Serikali ili iweze kuchukua hatua.

Alisema kunapokuwa na bidhaa feki sokoni, kampuni zinashindwa kushindana na kusababisha kupunguza wafanyakazi, hali ambayo baadaye kampuni huja kulaumiwa kwa kutoajiri watu.

Tunataka vitu halisi tu! Bandia hapana.

Friday, 10 June 2016

Disk gan nzuri zaidi?

Hard Drives (Disk) gani nzuri na imara zaidi? Angalia hapa kufahamu.

Toshiba, Seagate au WDC (Western Digital) haya ndio makampuni yanayoongoza kwa kutengeneza harddrives (diski hifadhi) duniani kwa sasa. Kampuni ipi inatengeneza diski hifadhi imara na inayodumu kwa muda mrefu angali orodha hii kutoka Blackblaze.

Cheki hapa orodha kamili ya viwango vya hard drives kama zilivyopimwa kwa muda wa masaa bilioni 1

Kwa kuwa makampuni mengi ya tech hayapendi kutoa data za kufeli kwa baadhi ya bidhaa zao, ni ngumu kutambua bidhaa zipi ni bora zaidi ya nyingine.

Kwa mfano makampuni yanayotengeneza bulb (taa) kwa kiasi kikubwa wanalazimika kuharibu au kutoruhusu bulb nyingi kuingia sokoni kwa kuwa zipo chini ya kiwango. Lakini hata siku moja hutowasikia wakilisema hili hadharani.

Kwa kuangalia matokeo haya utaona hard drives kutoka kampuni ya HGST kiwango kidogo cha ubora ukilinganisha na Hard drives kutoka katika kampuni ya Western Digital na Toshiba.

Thursday, 9 June 2016

BAJETI 2016/2017

BAJETI YA SERIKALI 2016/2017

SERIKALI imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53, ambayo nguvu kubwa imewekwa katika kukusanya mapato kwa kulinda viwanda vya ndani na kubana matumizi ya serikali ili kuelekeza sehemu kubwa ya matumizi katika maeneo ya vipaumbele.

Katika bajeti hiyo, bidhaa za lazima zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru wa barabara na maji ya kunywa, havijaguswa huku bidhaa za starehe kama bia, sigara, soda, juisi na nyingine kama nguo za mitumba, huduma za kupanga nyumba na uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa kodi, huku kiinua mgongo cha wabunge, kufutiwa msamaha wa kodi.

Aidha, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ikiwemo mapato ya taasisi za udhibiti kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Mafuta (EWURA), Shirika la Viwango (TBS), Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine za udhibiti, sasa yatapelekwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo mahitaji yao ya fedha yatatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, badala ya kujigawia kutokana na bakaa ya mapato waliyokusanya.

Aidha, maduka ya kutoa huduma katika majeshi, yamefutiwa kodi rasmi na badala yake, Serikali inajipanga kuongeza posho kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao, huku taasisi za umma na ofisi zote za Serikali, zikipigwa marufuku kufanya biashara na mzabuni asiyetumia mashine za kodi za kielektroniki (EFD’s).

Kodi juu 

Katika bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi ni pamoja na vinywaji baridi, kutoka Sh 55 kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa forodha katika maji ya matunda (juisi) yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa nchini, ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka 11 kwa lita. Juisi zinazotokana na matunda ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru wake pia umepanda kutoka Sh 200 kwa lita hadi Sh 210 kwa lita.

Bia, vilevi, mvinyo 

Kwa upande wa bia, serikali imependekeza bia inayotokana na nafaka ya hapa nchini, ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru upande kutoka Sh 409 kwa lita mpaka 430.

Bia zingine, ushuru wake pia umepanda ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729 kwa lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu, ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita mpaka Sh 534.

Kwa upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu zilizolimwa nchini kwa kiwango cha asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka Sh 192 kwa lita mpaka Sh 202.

Ushuru wa mvinyo unaotengenezwa na zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali, havikuachwa nyuma maana ushuru umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.

Sigara 

Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya hapa nchini kwa kiwango angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi Sh 11, 854 kwa kila sigara 1,000.

Kwa upande wa sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa kila sigara 1,000.

Sigara zenye sifa tofauti na hizo, ambazo hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya ndani, ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285 hadi Sh 50,700 kwa kila sigara 1,000.

Katika tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa kuwa sigara, ushuru wake umeongezeka kutoka Sh 24,388 hadi Sh 25,608 kwa kilo huku ushuru wa sigara aina ya Sigar ukibaki kuwa asilimia 30.

Vilainishi, gesi asilia, simu juu!

Katika mafuta ya kulainisha mitambo, ushuru umepanda kutoka Sh 665.50 kwa lita hadi Sh 699 kwa lita, huku ushuru wa grisi za kulainisha mitambo, ukipanda kutoka senti 75 kwa kilo, hadi senti 79 kwa kilo.

Gesi asilia pia ushuru umepanda kutoka senti 43 kwa futi za ujazo mpaka senti 45 kwa futi za ujazo.

Kuhusu viwango vya ushuru wa kuhamisha fedha kwa kutumia simu, serikali imependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10, kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu, katika kutuma na kupokea fedha, badala ya ushuru huo kutozwa tu katika kutoa fedha.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, kwa utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya wa kuhamisha sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.

Ulaji wa wabunge, hisa

Kwa upande wa kiinua mgongo cha wabunge wakati wa kustaafu, sasa kitatozwa kodi kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa.

Aidha, mapato yote yatokanayo na hisa katika kampuni mbalimbali sasa yatatozwa kodi, baada ya kufutwa kwa msamaha kwa waliokuwa wakimiliki hisa chini ya asilimia 25.

Kodi ya mishahara 

Katika kodi inayokatwa katika mishahara (P.A.Y.E), imepunguzwa kutoka asilimia 11 mpaka tisa kwa wafanyakazi wanaopata mshahara wa kuanzia Sh 170,000 lakini hauzidi 360,000. Kwa wanaopata zaidi ya 360,000 lakini haizidi 540,000, watakatwa Sh 17,100 pamoja na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.

Kabla ya hapo walikuwa wakikatwa Sh 20,900 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh 360,000.

Wanaopata zaidi ya Sh 540,000 lakini haizidi Sh 720,000, watakatwa Sh 53,100 pamoja na asilimia 25 ya kiasi kinachozidi 540,000.

Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 56,900 na hiyo asilimia 25 ya kiasi kilichozidi 540,000. Kwa wanaopata zaidi ya Sh 720,000 wao watakatwa Sh 98,100 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Sh 720,000.

Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh 101,900 pamoja na asilimia 30 ya kiasi kilichozidi Sh 720,000.

Kodi za nyumba 

Serikali pia imependekeza malipo ya kupanga nyumba, nayo yatozwe kodi ambayo haikuweka kiwango, ila imependekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato, apewe mamlaka ya kukadiria kiwango cha chini na cha juu cha mapato yapatikanayo na pango ili yatozwe kodi.

Kodi za nyumba, usajili magari, pikipiki 

Mbali na mapato ya kodi za nyumba, Serikali imependekeza kupandisha ushuru wa kusajili magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa kila gari na kutoka Sh 45,000 hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.

Kwa watumiaji wa namba binafsi za magari, ada sasa itapanda kutoka Sh milioni 5 kila baada ya miaka mitatu mpaka Sh milioni 10.

Kodi ya majengo 

Aidha, kodi za majengo sasa hazitakusanywa na halmashauri, badala yake TRA ndiyo inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria, kukusanya, kuhifadhi na kuiwakilisha katika halmashauri husika.

Mbali na TRA kupewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, serikali pia imependekeza kupunguza misamaha ya kodi za majengo ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.

Ulindaji wa Viwanda 
Saruji aina ya (HS Code 2523.29.00) zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ushuru wake wa forodha umepandishwa kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35 ili kulinda saruji inayozalishwa nchini dhidi ya ushindani wa bei ya saruji kutoka nje ya nchi.

Kwa bidhaa za chuma ikiwemo mabati kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, nazo ushuru umetoka asilimia 0 mpaka 10, ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini, huku bidhaa za nondo kutoka nje nazo zikipandishwa kodi kutoka asilimia 10 mpaka 25, kwa nia ya kulinda viwanda vya ndani.

Nyavu za kuvua samaki kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushuru wake umepanda kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 huku vichujia vya vilainishi na petroli kutoka nje ya nchi vikiongezwa ushuru kufikia asilimia 25 kutoka asilimia 10, ili kulinda bidhaa za ndani.

Sukari, ngano, mitumba, mafuta ya kula 

Katika sukari, serikali imekusudia kupunguza msamaha wa kodi na hivyo waagizaji wa bidhaa za sukari kutoka nje watalazimika kuanza kulipa ushuru wa asilimia 15 kutoka asilimia 10, huku ikitarajiwa kuongezeka zaidi na kuwa asilimia 20 mwaka 2017/18 na asilimia 25 mwaka 2018.19, ili kulinda viwanda vya ndani.

Kwa upande wa ngano kutoka nje, ushuru umepunguzwa kutoka asilimia 35 mpaka 10, kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki hazina uwezo wa kuzalisha kulingana na mahitaji.

Kwa upande wa nguo na viatu vya mitumba Serikali imepandisha ushuru kutoka dola za Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4 kwa kilo, kwa nia ya kudhibiti nguo hizo lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia uingizaji wake.

Kwa upande wa mafuta ya kula kutoka nje nayo ushuru umepanda kutoka asilimia 0 mpaka 10 kwa mafuta ghafi ya kula, ili kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta na viwanda vya ndani.

Tozo za pamba, kahawa, korosho

Miongoni mwa tozo zilizofutwa kuondoa kero kwa wananchi ni mchango kwa kila kiwanda cha kuchambua pamba wa Sh 450,000 na ada ya vikao vya halmashauri wakati wa kujadili wafanyabiashara wa pamba ya Sh 250,000.

Kwa upande wa kahawa, Serikali imefuta ada ya leseni ya kusindika kahawa ya dola za Marekani 250, huku ushuru wa kusafirisha korosho wa Sh 50 kwa kilo, ukifutwa.

Tozo zingine zilizofutwa katika korosho ni ushuru wa chama kikuu cha ushirika Sh 20 kwa kilo, gharama za mtunza ghala Sh 10 kwa kilo, kikosi kazi cha kufuatilia masuala mbalimbali Sh 10 na makato ya unyaufu.

Pia Serikali imepanga kuendelea kufuta tozo nyingine zinazokatwa na halmashauri, wakala na mashirika katika mazao ya wakulima, baada ya kufanya tathmini za kina.

Maduka kambi za jeshi 

Serikali imependekeza kufuta msamaha wa kodi uliokuwa ukitolewa katika maduka na migahawa maalumu kwa ajili ya askari wa majeshi, kutokana na msamaha huo kutumiwa vibaya na kupoteza mapato ya serikali na badala yake, askari watapata posho mpya juu ya posho ambazo wamekuwa wakipewa.

Toa maoni yako!

Tuesday, 7 June 2016

Shikamoo China!

China yatengeneza darubini kubwa zaidi kwa ajili ya kuchnguza mambo ya anga duniani.

Serikali ya China inamalizia mradi mkubwa wa kutengeneza darubini kubwa zaidi duniani itakayofanya kazi ya kuchunguza mwenendo wa mambo ya anga na nyota.

Darubini hiyo (telescope) ina ukubwa wa mita 500 na inatarajiwa kuwa kubwa mara mbili zaidi ya darubini ya sasa inayoongoza kwa ukubwa.

Kazi kubwa ya kituo hicho itakuwa ni kuchunguza kiasi cha gesi ya hydrogeni ambacho kinasemekana ndio mwanzo wa maisha duniani. Pia darubini hiyo itachunguza uwezekano wa kuwepo kwa maisha na viumbe huko angani na kuchunguza mienendo ya nyota zinazoenda kasi zijulikanazo kama pulsar.

Inaonekana uchina inataka kuingia rasmi kwenye ushindani wa sayansi za mambo ya anga na mataifa kama Marekani na Urusi.

https://www.youtube.com/watch?v=a_7SBglFfik&feature=youtube_gdata_player

VR Technology.

Ifahamu teknolojia ya Virtual Reality (VR) inayotikisa ulimwengu kwa sasa.

Kama wewe ni mmoja wa watu wanaofuatilia mambo ya teknolojia na habari utakuwa sio mgeni sana na huu msamiati unaotajwa kila kukicha katika mitandao na vyombo vya habari.

Virtual Reality au VR kama inavyotamkwa na watu wengi imepata umaarufu sana katika miaka ya hivi karibuni tofauti na ukongwe wa teknolojia hii.

Kampuni ya Nintendo ya Japani ndio ilikuwa kampuni ya kwanza kuleta teknolojia hii katika uso wa dunia katika miaka ya 70. Haikupata umaarufu mkubwa japo iliendelea kutumika katika maeneo mengi hasa ya elimu ya urubani na upasuaji.

Wanafunzi walioukuwa wakichukua mafunzo ya urubani katika vyuo mbali mbali walitumia VR ili kupata radha au muonekano ule ule uliokuwa katika mzingira halisi. Wanafunzi wa masuala ya uuguzi na udaktari pia wametumia sana teknolojia hii katika mafunzo yao.

Kwa sasa hali imekuwa tofauti kabisa, lengo la wanasayansi kuifanya teknolojia hii kuwa sehemu ya burudani linaonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Kwa sasa VR inatumika katika majumba ya sinema, sehemu za kucheza magemu na katika burudani nyingine nyingi.

VR ni nini hasa?
Hii ni teknolojia inayohusisha kuvaa kisanduku kilicho na matundu mawili usawa wa macho, kupitia matundu hayo unaweza ukaangalia muvi, kucheza magemu na mambo mengine mengi kama ukiwa katika ulimwengu halisi. Kupitia VR unaweza ukatembelea jangwa la Sahara, kuvuka mito mikubwa, kupambana na majitu ya ajabu. Kwa kifupi VR ni teknolojia inayokuwezesha kuota ndoto zako ukiwa macho.

Hayo yote yanawezeshwa na kompyuta au simu yenye uwezo wa kuzalisha picha zinazoonekana katika kisanduku hicho. Facebook wameifanya teknolojia hii kupata umaarufu tena kwa kuachia visanduku vya VR vijulikanavyo kama Oculus ambavyo kwa sasa vinatumika sana.  Kampuni za Sonny, Google na Samsung nao wameungana na Facebook katika hili.

Faida za Virtual Reality
VR zinafaida nyingi katika ulimwengu wa sasa ila hapa nitajaribu kuelezea chache kati ya hizo.
Elimu; Majeshi na vyuo mbalimbali vimekuwa vikitumia teknolojia hii muda sasa katika kufundishia hasa masomo yanayohitaji mazoezi ya kutosha na ya hatari.

Gaming ; Wapenda magemu wamepata teknolojia sahihi katika kuleta msisimko wa mchezo kwa kushiriki moja kwa moja katika mchezo husika. Fikiria unakimbizana na Usain Bolt katika mbio za mita 100 ndani ya VR.

Design ; Kupitia VR wasanifu majengo wanapata kazi rahisi ya kujua nini wataenda kufanya kabla hata ya kitu chenyewe kukamilika.

Porn: Asilimia 35 ya internet ni ngono, nadhani hapa umeelewa.

Hasara za VR
Kwa kiasi kikubwa teknolojia hii inamadhara sana katika mahusiano ya mtu na mtu, fikiria mpo kwenye ukumbi na wote mmevaa visanduku vya VR.  Au upo kwenye daladala huku unajisanduku cha VR usoni.

Nini kifanyike?
Kwa matumizi ya kielimu na burudani VR ni kitu kizuri sana, ila inapaswa watu wafahamu kwa undani teknolojia hii kabla ya kuanza kuitumia. Pia kwa watoto hasa wanaosoma ni vizuri kuwapa maelezo mazuri kabla ya kuwanunulia vifaa hivi.

World Pasword Day

WorldPasswordDay: Orodha ya Password 25 ambazo hutakiwi kutumia.

Katika kuadhimisha siku ya Password duniani leo tunakutea password 25 ambazo hutakiwi kutumia kabisa katika akaunti zako kwa mujibu wa SplashData.

Worst-passwords
Ngoja tukumbushane wale wanaopenda kutumia password rahisi kama majina yao, 1234, 12345678 au qwertyui au majina ya sehemu wanazotokea. Aina hizo za password hazifai kabisa kutumika katika akaunti zetu.

Hebu tuangalie orodha ya password mbaya zaidi ambazo hazifai kutumiwa kwa sababu zimekuwa rahisi zaidi kudukuliwa na wadukuzi. Unaweza ukapita hapa ili kuangalia mbinu za kutengeneza password zenye usalama zaidi.

Pata software za bure!

Ninite.com, sehemu salama ya kupata softwares za bure za Windows

Ninite.com ni sehemu pekee unayoweza kudownload na kuinstal software za Windows bure na kwa usalama zaidi kwa pamoja. Utofauti wa ninite.com ni uwezo wa kudownload na kuinstal software nyingi kwa wakati mmoja yenyewe bila kumsumbua mtumiaji wa Pc kuclick Next, Next…

ninite
Tunapobadilisha Windows au tunapohamia toleo jingine la Windows (Upgrade) huwa tunapata tabu sana katika kutafuta installer za software zote za msingi kama Google Chrome, Adobe reader, Skype, Mozila Firefox, VLC media player na kuziinstall mojamoja mpaka tunaporidhika. Kwa kompyuta moja inaweza isiwe shida sana lakini ni tofauti kama una kompyuta zaidi ya moja, kuzidownload na kubonyeza Next, next… ni jambo la kuchosha kidogo.

Hapa ndipo ninite.com inapoingia, ninite itakusaidia kuinstall application zote za muhimu bila tabu wala usumbufu wowote ule. Katika mtandao (tovuti) ya ninite utaona maelekezo jinsi kuinstal application unazotaka, hakuna kitu kigumu zaidi ya kuchagua application au software unazotaka na kuinstall bila tabu. Ninite yenyewe haitachagua offer au tools bars zinazokuja na baadhi ya installer hivyo kukupa usalama zaidi.

kufahamu zaidi tembelea blog yangu!

Dr Tulia awatetea Ukawa.

Dk Tulia alazimika kuwatetea Ukawa

Dodoma. Licha ya wabunge wa upinzani kususia vikao anavyoendesha na kutaka kumng’oa kwenye wadhifa wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amelazimika kuwatetea na kuwaeleza wabunge wa CCM kuwa, ili kuwakata posho wanaosuasa vikao kuna haja ya kurekebisha sheria.

Dk Tulia alilazimika kutoa ufafanuzi huo jana, baada ya wabunge wengi wa CCM kuomba mwongozo wa kutaka wabunge wa Ukawa, waliotangaza kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika wakatwe mshahara na posho.

Dk Tulia alikuwa akitoa majibu ya miongozo iliyoombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy ambao walitaka kuelezwa kwa nini wabunge hao wamekuwa wakiingia na kutoka na kutaka wakatwe posho na mishahara yao.

Wakati hayo yakijiri, Spika wa Bunge, Job Ndugai anakusudia kuwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ombi la wabunge wa upinzani la kumng’oa naibu huyo.

Hatua hiyo ya Spika inakuja baada ya Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya kuwasilisha  taarifa ya kusudio la kuleta bungeni hoja ya kumuondoa madarakani Dk Tulia, Juni Mosi mwaka huu.

Wednesday, 1 June 2016

Mgomo wa UDSM.

Walioandaa mgomo UDSM kukiona!

Dar es Salaam. Wanafunzi walioandaa mgomo wa jana Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) huenda wakakumbwa na hatua za kinidhamu kwa kosa la kukikuka sheria ndogo ya Chuo kwa kuandaa mkusanyiko pasipo kibali cha Menejimenti.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo taaluma Florens Luoga amesema kuwa hadi  sasa mamlaka za nidhamu chuoni hapo zinendelea na uchunguzi kubaini nani alihusika na ni kwa namna gani na baada ya hapo hatua za kinidhmu zitafuata.

“Taratibu na sheria ndogo za chuo haziruhusua mtu kuandaa mkusanyiko ambao haujaidhinishwa na menejimenti na kimsingi taratibu hizo lazima ziheshimiwe ili kuzifanya kuendelea kuwa imara hivyo tunasubiri ripoti ya walio husika endapo itaonesha  kuwa wanamakosa basi watachukuliwa hatua za kinmidhamu,” amesema Luoga.