Tuesday, 7 June 2016

Dr Tulia awatetea Ukawa.

Dk Tulia alazimika kuwatetea Ukawa

Dodoma. Licha ya wabunge wa upinzani kususia vikao anavyoendesha na kutaka kumng’oa kwenye wadhifa wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amelazimika kuwatetea na kuwaeleza wabunge wa CCM kuwa, ili kuwakata posho wanaosuasa vikao kuna haja ya kurekebisha sheria.

Dk Tulia alilazimika kutoa ufafanuzi huo jana, baada ya wabunge wengi wa CCM kuomba mwongozo wa kutaka wabunge wa Ukawa, waliotangaza kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika wakatwe mshahara na posho.

Dk Tulia alikuwa akitoa majibu ya miongozo iliyoombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy ambao walitaka kuelezwa kwa nini wabunge hao wamekuwa wakiingia na kutoka na kutaka wakatwe posho na mishahara yao.

Wakati hayo yakijiri, Spika wa Bunge, Job Ndugai anakusudia kuwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ombi la wabunge wa upinzani la kumng’oa naibu huyo.

Hatua hiyo ya Spika inakuja baada ya Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya kuwasilisha  taarifa ya kusudio la kuleta bungeni hoja ya kumuondoa madarakani Dk Tulia, Juni Mosi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment