Sunday, 28 February 2016

Demokrasia barani Africa.

Kwa ufupi

Pamoja na tafsiri nyingi zilizowahi kutolewa na kufundishwa, utekelezaji wa dhana ya demokrasia hapa Afrika una tafsiri maalum kutoka kwa vyama vilivyokaa madarakani muda mrefu au wakuu wa nchi waliosalia madarakani kwa muda mrefu.

Habari
SUNDAY, FEBRUARY 28, 2016
DARUBINI YA MTATIRO :
Demokrasia ya Afrika ni uhuni
mtupu!

Julius Mtatiro
Wengi wetu walipokuwa shule za msingi na sekondari walisikia na kulijua neno demokrasia kwa mara ya
kwanza likitajwa na kupewa maana zake.

Moja ya maana za demokrasia ni “utawala wa watu kwa ajili ya wao wenyewe...” na tena maana nyingine ni “utawala unaowekwa na watu kwa
kufuata misingi waliokubaliana”.

Pamoja na tafsiri nyingi zilizowahi kutolewa na kufundishwa, utekelezaji
wa dhana ya demokrasia hapa Afrika una tafsiri maalum kutoka kwa vyama vilivyokaa madarakani muda mrefu au
wakuu wa nchi waliosalia madarakani kwa muda mrefu.

Kuna demokrasia mbili Afrika, ile ya watawala na ya watawaliwa. Ya watawala haitabiriki na inakuwapo pale wanaposhinda uchaguzi kupitia njia mbalimbali na hasa kwa msaada wa vyombo vya dola, mabavu, rushwa, vitisho, mifumo ya uongozi ya kiupendeleo na tume za uchaguzi zinazoongozwa na wao wenyewe.

Demokrasia hii ya watawala
imeonekana Zanzibar kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 watawala walipoona Maalim Seif Sharif Hamad anaelekea kushinda uchaguzi wakazuia
kwa nguvu matokeo yasiendelee kutangazwa na kisha yakafutwa na ‘mtu’ mwenye dhamana ya kuisimamia tume kwa kufuata kanuni za uchaguzi, sheria na katiba ambavyo hata mara
moja havimpi yeye au tume nzima mamlaka ya kufuta matokeo ya jumla ya uchaguzi na ambayo yamethibitishwa na ngazi za wasimamizi wa uchaguzi.

Matokeo yaleyale yaliyomzuia Maalim Seif kuwa rais wa Zanzibar ndiyo yakampaisha Rais John Magufuli kutangazwa kuwa Rais wa Tanzania.

Kidemokrasia (Demokrasia ya
Tanzania) kwa tafsiri ya dola na chama kinachoongoza dola ni pale ambapo wagombea wa CCM wangelikuwa wanaongoza wote, lakini pia bila aibu aliposhindwa mmoja wakashindwa kujibaraguza ilimradi wazuie matokeo yote ya Zanzibar kwa chaguzi zote
(urais wa Jamhuri na ule wa Zanzibar) na kwa hivyo uchaguzi wa marudio
unaokwenda kufanyika Zanzibar (huku vyama vyenye nguvu kama CUF vikiwa vimeususia) ungelifanyika kwa nafasi zote za urais wa Jamhuri na ule wa Zanzibar.

Ndiyo kusema hadi leo wakati fukuto la Zanzibar linaendelea Jakaya Kikwete angepaswa kuwa madarakani huku
John Magufuli (aliyekuwa anaongoza kura za urais wa Jamhuri wakati matokeo ya Zanzibar yanafutwa) akisubiri apigiwe kura upya Zanzibar
kabla ya kutangazwa mshindi wa jumla wa uchaguzi wote.

Kwa vyama vilivyoongoza Afrika muda mrefu demokrasia ni jambo la upande mmoja, ni jambo la wao wanataka kupata nini, ni jambo la wanachokipata
kinawatosha kiasi gani!

Watawala wa Afrika huitafsiri demokrasia yao na kuilazimisha ikubalike hivyo ilivyo kwa kadri watakavyoamua, na hapo
ndipo bara hili linakwama.

Kwenye shule zetu watoto wanaendelea kufundishwa demokrasia ni maamuzi
ya wananchi na wengine wanadhani jambo hilo ni dhahiri, kwenye utekelezaji demokrasia ya Kiafrika ni
tofauti na kile kinachofundishwa na
labda kinachofanywa na wenye demokrasia wenyewe, huko nchi za Magharibi.

Mwalimu Kitila Mkumbo (Profesa) mara kadhaa amepata kuandika juu ya
“dhana ya demokrasia ya Afrika” na amekuwa akihoji ikiwa kuna haja ya
Afrika kuendelea na demokrasia hiyo ya maigizo badala ya kukaa chini na
kuamua moja na hata kuanzisha demokrasia ya Afrika na kuijulisha dunia “hii ndiyo demokrasia yetu!”

Kitila anaongelea dhana pana ya unafiki mkubwa unaofanywa na viongozi wa Afrika kuanzia kwenye ngazi ya chama kimoja kimoja (kilichoshika dola na visivyoshika dola) na ngazi ya nchi ambapo vyama vyote
hukutana na kushindana ili kimoja kipate ushindi wa jumla.

Hii ni wiki ambayo nchini Uganda kumekuwa na gumzo la Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni na wakati
wananchi wa kawaida wanaimba mabadiliko wayatakayo, vyombo vya
dola na rais aliyeko madarakani,
Yoweri Museveni wanasimamia kile
wanachokiamini kama “ni lazima Museveni aendelee kutawala”. Katika wiki ya mwisho ya uchaguzi, kiongozi
mkuu wa upinzani nchini Uganda, Kiza Besigye, alikamatwa na kushikiliwa mara tatu.

Mara ya mwisho ni siku ya
uchaguzi yenyewe tena akiwa katika mizunguko ya kufuatilia mienendo ya uchaguzi. Kiongozi mwingine wa
upinzani, Amama Mbabazi naye aliwekwa jela ya nyumbani kwake siku
ya uchaguzi.

Haya yote yakifanywa na majeshi ya Uganda yakishirikiana na walinda
usalama wengine, hii ndiyo demokrasia ya Afrika. Museveni hana mpango wa
kuondoka madarakani na kwake yeye na wanaonufaika moja kwa moja na utawala wake ‘demokrasia sahihi ni
yeye kutawala!”

Ukihamia pale Burundi utakumbana na matatizo makubwa, Pierre Nkurunziza
amekatalia madarakani, alifanya uchaguzi wa upande moja akajihalalisha kuendelea kuwa mtawala wa Burundi. Kwa Nkurunzinza, tafsiri
ya demokrasia ni yeye kuendelea kuitawala Burundi.
Mamia ya watu waliouawa kwenye machafuko yaliyoongozwa na vyombo
vya dola ili kuwanyamazisha
wapinzani wa Nkurunziza, hakujali, kwake demokrasia ni “kusalia madarakani” hata kama watu wanakufa!

Majirani zetu Wanyarwanda wanapita kwenye yaleyale, Rais Paul Kagame anaamini hakuna Mnyarwanda mwenye uwezo wa kuongoza nchi hiyo,
amekaa madarakani miongo miwili na bado yumo tu, yeye tu! Vyama vilivyosajiliwa pale Rwanda vinafanya kazi kama wakimbizi.

(Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya Kijamii na Kisiasa (Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB) +255787536759,

juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments:

Post a Comment