Wednesday, 24 February 2016

NGELI ZA KISWAHILI

Kufahamu ngeli za Kiswahili kunamwezesha mwanafunzi kuelewa upatanisho wa kisarufi katika sentensi, kutambulisha maumbo ya umoja na uwingi pia kufahamu uhusiano wa Kiswahili na lugha zingine.

Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi yanayofanana.

Kufahamu ngeli za Kiswahili kunamwezesha mwanafunzi kuelewa upatanisho wa kisarufi katika sentensi, kutambulisha maumbo ya
umoja na uwingi pia kufahamu uhusiano wa Kiswahili na lugha zingine.

Ngeli ya A–WA hutumika kurejelea viumbe vilivyo hai (wanyama na watu). Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwa sauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi.

Hata hivyo baadhi ya majina huchukua miundo tofauti.
Mifano; mgonjwa - wagonjwa, mchungaji - wachungaji, mwizi-wezi, mtu- watu.
Muundo ulio tofauti na maelezo hapo juu ni kama mbuzi-mbuzi, kwale - kwale  nyati - nyati kifaru – vifaru.

Ngeli ya LI-YA husimamia nomino zenye miundo mbalimbali. Licha ya majina ya vitu visivyo hai, ngeli hii pia hutumika kwa majina yote katika hali ya ukubwa (yakiwamo ya watu au wanyama). Majina mengi huanza kwa JI- au J- kwa umoja na hubadilishwa kuanza
na MA- au ME- kwa wingi.

Majina mengine
ambayo huanza kwa sauti nyingine kama vile /b/, /d/, /g/, /k/, /z/ n.k ambayo huwekwa katika wingi kwa kuongeza kiungo MA-
Mifano; jimbo - majimbo, jicho - macho, jiko - majiko, jino - meno, maua, umbo - maumbo,
bati - mabati.

Ngeli ya KI - VI hurejelea vitu visivyo hai ambavyo majina yao huanza kwa KI- au CH-
(umoja) na VI- au VY- (wingi).
Mifano; kijiko - vijiko, kikapu - vikapu, kioo- vioo, choo - vyoo, chumba - vyumba, chuma -
vyuma, chungu - vyungu.

Ngeli ya U - I
huwakilisha nomino za vitu visivyo hai na ambavyo majina yake huanza kwa sauti M -
(umoja).
Mifano; mfupa - mifupa, mtambo - mitambo,
mfuko – mifuko.
Ngeli ya U - ZI hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI-
kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi. Mifano; ufunguo - funguo, ukuta – kuta.

Majina ya silabi mbili katika ngeli hii huongezwa NY katika uwingi. Mifano; uzi - nyuzi, uso – nyuso.

Ngeli ya I - ZI hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (wingi).

Aghalabu haya ni majina ya vitu ambayo huanza kwa sauti N, NG, NY, MB, n.k
Mifano; nyumba - nyumba, nguo - nguo, mbegu - mbegu, nyasi - nyasi, nyama – nyama.

Ngeli ya U - YA hujumuisha nomino ambazo zina kiambishi awali u-katika umoja na ma-
katika uwingi. Mifano; unyoya - manyoya.

Ngeli ya KU huwakilisha majina yanayotokana na vitenzi kwa vitenzi vinavyoanza na ku-
(huitwa vitenzi jina). Mfano Kusoma kwetu kumetusaidia, Kusema uongo kumemponza.

Ngeli ya mahali PA - KU – MU. Ngeli ya PA hurejelea mahali maalumu, padogo au palipo
wazi. Ngeli ya KU hurejelea mahali fulani kwa jumla au eneo fulani. Ngeli ya MU - hutumika kurejelea mahali ndani ya kitu kingine kama vile ndani ya nyumba, shimo n.k.

Ngeli za mahali hubaki vivyo hivyo katika umoja na wingi Hivyo, mwanafunzi anaweza kufanya mazoezi kadiri awezavyo kwa kutunga sentensi umoja na uwingi kwa kutumia neno au kitenzi jina ili kubaini kundi husika la neno au maneno.

Mwandishi ni mtaalamu wa
Kiswahili.chanzo.KISWAHILI KWA WANAFUNZI: Ngeli tisa za Kiswahili na upatanisho wa kisarufi - Makala - mwananchi.co.tz

Tujifunze kiswahili yetu!

No comments:

Post a Comment