Thursday, 10 March 2016

EZEKIEL WENJE

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje 

Kahama/Mwanza. Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje (pichani) anakusudia kuita mahakamani zaidi ya mashahidi 693 kupinga ushindi wa mbunge wa sasa, Stanslaus Mabula (CCM).

Wakili wa Wenje, Deya Outa aliieleza mahakama kuwa mashahidi hao ni pamoja na waliokuwa wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Tunatarajia kuita mahakamani mashahidi wasiopungua 693 kuthibitisha madai yetu, kulingana na mahitaji ya hoja tunazotaka kuzithibitisha mahakamani,” alidai wakili Outa.

Pande zinazohusika kwenye shauri hilo namba 3 la mwaka 2015, juzi ziliweka wazi hoja wanazokubaliana na zile wanazobishania kabla ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo anayesikiliza shauri hilo kuihairisha hadi Machi 14, mwaka huu, itakapoanza kusikilizwa mfululizo.

Pamoja na Mabula, wadaiwa wengine katika shauri hilo linalovuta umati wa wasikilizaji ni aliyekuwa msimamiza wa uchaguzi Nyamagana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kutokana na wingi wa mashahidi na muda wa mwaka mmoja uliowekwa kisheria wa mashauri ya uchaguzi kusikilizwa na kuamuliwa, wakili Outa alisema iwapo muda huo utaisha kabla hawajamaliza kutoa ushahidi wao, wataiomba mahakama kuwaongezea muda wa ziada.

Lembeli apeta

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kahama mjini kupitia Chadema, James Lembeli ameruka kihunzi kingine baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga inayosikiliza shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo kutupilia mbali pingamizi la mashahidi wa mlalamikaji lililokuwa limewekwa na mawakili wa upande wa mshitakiwa.

Akitoa uamuzi huo jana mjini Kahama, Jaji Moses Mzuna alisema ni kinyume cha sheria na wala siyo haki kuzuia mashahidi wa mlalamikaji kutoa ushahidi wao, hivyo ni vyema wakatoa na haki ikatendeka.

Uamuzi huo ulifuatia mvutano mkali wa kisheria uliotokea Machi 4, mwaka huu, baina ya mawakili wa upande wa utetezi na wakili wa mlalamikaji ambapo Jaji Mzuna aliahirisha shauri hilo, hadi alipolitolea uamuzi jana asubuhi.

Katika mvutano huo, mawakili wa utetezi Anthony Nasimire, Denis Kahangwa na Castuce Ndamugoba walipinga mashahidi wa Lembeli kutoa ushahidi wao kwakuwa walikiuka sheria inayowataka kuwasilisha viapo vyao mahakamani ndani ya saa 48, kabla ya shauri kuanza kusikilizwa.

Pia Jaji Mzuna alisema sheria hiyo ni mpya na kwamba haikujulikana kwake, kwa mawakili wa pande zote, na hata katika rejea za kimahakama nchini ndiyo maana hata mawakili wa utetezi wameiwasilisha wakati ushahidi umekwishaanza kutolewa.

Alifafanua kwamba sheria ya uchaguzi inaelekeza mlalamikaji kutoa ushahidi usioacha mianya ya mashaka, jambo ambalo pia mahakama iliona si vyema mashahidi walioandaliwa kuzuiliwa kutoa maelezo yao, hali itakayobana uwigo wa upatikanaji wa haki.

Kwa upande mwingine Jaji Mzuna aliikataa hoja ya wakili wa Lembeli, Mpale Mpoki kwamba muda wa kuandaa viapo haukuwepo kwa kuwa ilimchukua muda mwingi kuandaa shauri hilo, ambapo Jaji Mzuna alisema haikubaliki kisheria.

Hata hivyo alisema kuchelewa kwa Mpoki kupeleka viapo vya mashahidi hakuwezi kuwa sababu ya Lembeli kupoteza fursa ya kudai haki yake anayohisi alipokonywa, bali muda zaidi umetolewa wa kuandaa viapo hivyo.

Kufuatia hali hiyo Jaji Mzuna aliahirisha shauri hilo hadi Machi 15 mwaka huu ambapo mahakama itaanza kusikiliza maelezo ya mashahidi wa Lembeli waliokuwa wamesubiri uamuzi dhidi ya mvutano huo wa kisheria uliopinga mbunge huyo wa zamani wa jimbo la kahama asipeleke mashahidi wake mahakamani.

Wasira kusubiri uamuzi

Wapiga kura wa Bunda Mjini waliowasilisha maombi ya kuruhusiwa kukata rufaa nje ya muda, kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Ester Bulaya dhidi ya Steven Wasira, wamekumbana na kigingi kingine cha pingamizi.

Maombi hayo namba 25 ya mwaka 2016 yaliwasilishwa na wapiga kura Magambo Masato na wenzake watatu, wakiiomba mahakama hiyo iwaruhusu kukata rufaa nje ya muda baada ya kutupiliwa mbali na mahakama kuu.

Pingamizi hilo liliwasilishwa jana na wakili wa wajibu maombi wa pili na wa tatu, Paschal Malulu akiiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa kiapo kilichoambatanishwa ni batili kwa kuwa aliyeapa ni tofauti na aliyethibitisha.

“Haya makosa yaliyofanyika ni makubwa mno, kiasi cha kutokurekebishika, kwa sababu kiapo kimethibitishwa na wakili Constatine Mutalemwa huku aliyeapa ni wakili James Kahangwa,” alidai Malulu.

Alidai kiapo hicho kimekosa nguvu kisheria kwa mujibu wa sheria Na. 19 (1) (2), ni lazima kiwe na mambo ambayo mtu anaweza kuyathibitisha au kuyasimamia, hivyo hii sheria imekiukwa, kwa lugha nyingine kiapo kimekosa uthibitisho.

Malulu alidai kuwa kuna sheria inayosimamia kiapo wala siyo Katiba kwa ujumla wake, kama alivyoitaja Mutalemwa.

Jaji anayesikiliza shauri hilo, Rose Ebrahim aliahirisha shauri hilo hadi Machi 14, mwaka huu atakapolitolea maamuzi pingamizi hilo.    

No comments:

Post a Comment