MUUNGWANA BLOG / 25 minutes ago
Waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi Mwigulu Nchemba ameusimamisha uongozi wa chama cha wakulima wa miwa Tanzania (TASGA) baada ya kubaini kuwepo vitendo vya unyanyasaji.
Tuhuma nyingine ni kushindwa kuwasaidia wakulima wa miwa na kusababisha migogoro kati wakulima na kiwanda cha sukari cha Kilombero.
Akizungumza katika mkutano wa wakulima wa miwa wa bonde la Ruhembe waziri Mwigulu amesema serikali haiwezi kuvumilia viongozi wanaotumia madaraka yao kuwanyanyasa na kuwagandamiza wakulima.
Mwigulu ameagiza mkuu wa mkoa na uongozi wa wilaya kuwasimamia wakulima hao kuhakikisha wanapata uongozi wa muda ndani ya siku mbili huku akiwataka wawekezaji kuwalinda wakulima kimaslahi ili waweze kunufaika na rasilimali zilizopo nchini kwa kuzingatia masharti ya serikali.
Awali wakitoa kilio chao mbele ya waziri huyo, wakulima hao wamemwambia waziri kuwa pamoja na changamoto lukuki zinazowakabili mwenyekiti wao amekuwa kikwazo cha maendeleo ya wakulima wa Ruhembe ikiwa ni pamoja na kubadilisha katiba ya chama kwa lengo la kuendelea kubaki madarakani.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la mikumi mheshimiwa Joseph Haule ameshukuru ujio wa waziri wa kilimo kwani hali ya wakulima wa miwa wa bonde hilo ni mbaya kutokana na unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vyao pamoja na wawekezaji kwa kuwanyima haki wakulima wa miwa.
No comments:
Post a Comment