Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Ezekiel Olouch amesema upangaji matokeo ya kidato cha nne kwa mfumo wa divisheni uliofanywa na Wizara ya Elimu, ni batili na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anatakiwa kushtakiwa.
Mwalimu Olouch aliitoa kauli hiyo juzi kwenye kongamano la walimu Kitengo cha Wanawake Manispaa ya Dodoma kuwa, Profesa Dk Ndalichako anapaswa kushtakiwa.
Pia, alipinga suala la kutumbua majipu kwani linakwenda kinyume na haki za binadamu.
“Mambo mengi yanafanywa kwa pupa hasa yanayofanywa na manaibu waziri, na baadhi ya wakuu wa wilaya nchini,” alisema Mwalimu Olouch.
Kuhusu matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Februari, alisema kitendo cha waziri kuamua kufuta mfumo wa GPA na kurudisha divisheni, kilikuwa kizuri lakini aliufanya kwa kukurupuka.
Mapema mwaka huu akiwa mjini Dodoma, Profesa Ndalichako alitangaza kubadilisha mfumo wa matokeo kutoka GPA kurudi wa zamani wa divisheni ikiwa ni wiki chache kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo.
“Hapa tuelezane ukweli kwamba Ndalichako amevunja sheria na mimi ningekuwa na mtoto aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana, lazima ningemfikisha mahakamani haiwezekani kuwa na elimu ya kukurupuka, kitaaluma ni matokeo feki lakini kisiasa ni matokeo halali,” alisema Mwalimu Oluoch.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Waziri anaruhusiwa kubadilisha lakini lazima aaandike kanuni na mwongozo jambo alilodai halikufanyika.
Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Dodoma, Augustino Njamasi alimtaka chama kuendelea kupigania masilahi ya walimu ikiwamo madeni.
No comments:
Post a Comment