Friday, 4 March 2016

MBARAWA NA HALOTEL

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame  

Tanga. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kampuni ya simu za mkononi ya Halotel itachukuliwa hatua kwa kukiuka makubaliano ya kuunganisha mitandao kwenye shule tatu katika wilaya mbalimbali nchini.

Amesema badala yake imetoa ‘moderm’ ili kuziwezesha shule kupata mawasiliano ya intaneti, jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana baina ya Serikali na kampuni hiyo ilipokuwa ikiomba kibali.

Profesa Mbarawa amesema hayo leo, baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Tanga iliyotolewa na Katibu Tawala wa mkoa huo, Salim Chima.

“Hii siyo nchi ya ‘moderm’ hatuwezi kukubali, wakati wakiomba leseni waliahidi kuweka mtandao wa mawasiliano ya intaneti kwa kuunganisha katika mkongo (wa Taifa), lakini wao wametoa ‘moderm’,” amesema.

Waziri huyo ambaye yupo mkoani hapa kutembelea miundombinu ya sekta zilizo chini ya wizara yake, alisema hawezi kukubaliana na kile alichokiita udanganyifu, hivyo atakaporejea ofisini atashughulikia suala hilo kikamilifu.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwa waziri huyo na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi ilisema Halotel imetoa ‘moderm’ kwa shule za sekondari za Old Tanga, Mikanjuni na Maweni.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Katibu Tawala, Chima alimweleza waziri kuwa Mkoa wa Tanga umekusanya Sh7.1 bilioni msimu uliopita na kwamba, halmashauri zinazokusanya kwa mfumo wa kielektroniki ni sita kati ya 12.

Profesa Mbarawa aliwataka viongozi wa mkoa huo kusimamia ipasavyo ufungaji wa mfumo wa kielektroniki kwa kila halmashauri ili kukwepa udanganyifu unaoisababishia Serikali kupoteza mapato.    

No comments:

Post a Comment