Friday, 25 March 2016

IMANI THABITI YENYE TIJA.


Daktari Ahmed, mtaalamu wa ugonjwa wa kansa alikuwa na safari ya kwenda kushiriki mkutano wa muhimu mno katika mji mwingine tofauti na aliopo, mbali na kushiriki mkutano huo pia alikua akitarajiwa kutunukiwa tuzo ya umahili katika tafiti za kiafya.

Alikuwa ameutamani sana huo mkutano na alikuwa akihitaji kufika haraka iwezekanavyo. Amefanya kazi ya utabibu na utafiti kwa muda mrefu hivyo alijiona kweli anahitaji kupata tuzo ambayo alikuwa akiitarajia.

Hata hivyo baada ya masaa mawili ya kukaa angani katika ndege akielekea huko kwenye mkutano, ndege ilipata hitilafu na ikabidi itue katika airport iliyopo karibu.

Akiwa na hofu kwamba atachelewa mkutano, Daktari Ahmed akaenda mapokezi pale airport na kukuta kuwa ndege nyingine inayoenda huko anakoenda itaondoka pale baada ya masaa kumi.

Receptionist akamshauri kwama aazime gari na aendeshe mwenyewe mpaka huko anakoelekea kwani ilikuwa ni mwendo wa masaa matatu tu na gari.

Kwakuwa alikuwa hana chaguo jingine, alikubaliana na yule dada wa mapokezi kuazima gari ingawa alikuwa hapendi idea ya kuendesha gari kwa muda mrefu.

Aliazima gari na akaanza safari. Hata hivyo muda mfupi tu baada ya kuondoka hali ya hewa ilibadilika ghafla na kimbunga kikali kikaanza.

Mvua kubwa ikiyoambatana na ukungu ikamfanya apate sana tabu kuona mbele na akapotea barabara aliyokuwa anahitajika kwenda.

Baada ya masaa mawili ya kuendesha gari, akathibitisha kweli amepotea njia. Kuendesha katika mvua kubwa yenye upepo na kimbunga, huku akiwa na njaa na amechoka, ikamlazimu atafute nyumba yoyoye aulizie hapo ni wapi na apate kuelekezwa anakoelekea.

Baada ya muda kidogo hatimaye akaona nyumba ndogo ikiwa kando kidogo mwa barabara. Akaegesha gari pembeni akashuka na kwenda kugonga hodi mlangoni.

Mwanamke mwembamba na mzuri akamfungulia mlango. Daktari Ahmed akamuelezea tatizo lake na akamuomba yule dada kama anaweza akatumia simu yake kuwataarifu kule mkutanoni kilichompata.

Hata hivyo, yule dada akamwambia yeye hana simu wala kifaa chochote cha mawasiliano lakin akamuomba daktari aingie ndani asubiri hali ya hewa itulie vema. Akiwa na njaa, amelowa daktari alikubali kuingia ndani.

Yule mwanamke akampa daktari chai ya moto, na akamwambia anaomba aungane nae katika maombi.

Ambapo daktari alitabasamu na akasema yeye anaamini katika kufanya kazi kwa bidii na sio maombi. Hivyo akamwambia yeye aendelee tu.

Akiwa amekaa akiendelea kunywa chai taratibu, daktari alimwangalia yule mwanamke katika mwanga mdogo wa mishumaa akiwa anasali mbele ya kitu kama kitanda cha mtoto hivi.

Kila muda akimaliza kufanya sala, anaanza sala nyingine. Daktari akahisi labda huyu mwanamke anahitaji msaada fulani hvyo akamsubiri amalize kusali amuulize anasumbuliwa na nini.

Alipomaliza daktari alimuuliza yule mwanamke kuwa ni nini haswa anahitaji kutoka kwa Mungu? Na kama Mungu amemsikia maombi yake. Na akendelea kumuuliza kuhusu mtoto aliyepo katika kitanda ambae amelala hajitambui.

Mwanamke akampa tabasamu la huzuni na kumwambia kwamba mtoto aliyepo kwenye kitanda ni wake ambae anasumbuliwa na kansa kwa muda mrefu.

Na kuna daktari mmoja tu bingwa katika mji mwingine tofauti na huu anaitwa Daktari Ahmed ndio ana uwezo wa kumtibu mwanangu.

Lakini hapa unaponiona sina pesa ya kumtibia mwanangu wala nauli ya kunifikisha huko aliko Daktari Ahmed.

Ni kweli Mungu hajajibu maombi yangu, ila siku zote sikubali woga wangu uzidi imani yangu juu ya Mungu wangu.

Akiwa ameshtushwa na kushangazwa Daktari Ahmed alikuwa akitokwa na machozi, alijiambia kweli Mungu ni mkuu na akajaribu kuunganisha matukio.

Kulikuwa na tatizo katika ndege, nikakodi gari, nako mvua kubwa na kimbunga vikanifanya nipotee njia na kufika hapa.

Yote haya yametokea sio kwa bahati mbaya bali ni makusudi ya Mungu daktari afike hapa kupata nafasi ya kusaidia masikini kama huyu ambae hana pesa ila ana utajiri wa imani juu ya Mungu.

Daktari alijitambulisha kuwa yeye ndio Ahmed, na akakiri kumbe kweli Mwenyezi Mungu hujibu maombi.

Aliwachukua wote wawili na akaenda nao katika mji anakofanya kazi, alimpa matibabu yule mtoto na kwa kipindi kama cha miezi 8 yule mtoto alipona.

FUNDISHO
Sisi kama binadamu tunahitajika kukumbuka hatua hizi muhimu katika maisha.

1. Omba
2. Amini
3. Pokea
4. Toa

Nawatakia Pasaka  njema na Mwenyezi Mungu awabariki.

No comments:

Post a Comment